Saturday, September 29, 2012

Maisha kwanza, kesi baadae!


Kama kawaida, nilikuwa napata masimulizi ya hapa na pale katika saluni – na nilisimuliwa jinsi mama daktari wa kujitolea mgiriki alivyofariki dunia, jijini Dar, chanzo na mtiririko wa matukio.
Hii ni simulizi na si habari iliyothibitishwa. Kwa kifupi mama huyu mgiriki alikuwa anatembea Ali Hassan Mwinyi Road na vibaka walipita na gari na kuvuta begi lake la mgongoni (back pack) na kumburuza mita kadhaa na gari. Hatimaye walichukua begin a kumwacha huyu mama. Sehemu hii imethibitishwa – ni kweli ilitokea. Ila sasa nilichoendelea kusimuliwa ni kuwa wagiriki wenzake walihangaika tokea saa 12jioni hadi saa 2 usiku wakijaribu kupata form ya polisi – kwani bila hiyo fomu hupokelewi hospitalini. Walifika hospitali ya Aga Khan saa 2 lakini pamoja na kujitahidi kwa madaktari wenzake wagiriki (ambao waliamua kuingia katika harakati za kumwokoa) lakini mama huyu alifariki.
Katika simulizi hii yote kilichonisikitisha ni kuwa mtu anapopata ajali ni lazima apate fomu ya polisi kabla ya kutibiwa! Hii si sawa! Nimewahi kushauriwa na polisi afisa mmoja na hata leo saluni walinishauri “Ukikuta mtu kagongwa barabarani, usihangaike kusimama. Utasumbuliwa na unaweza ukakuta kesi inakugeuka” Hii haiingi akilini! Hivi kweli tumefikia hatua ya kuacha binadamu wenzetu wakivuja damu barabarani kwa sababu ya sheria mbovu? Hivi kweli tumeshindwa kushinikiza bunge, serikali nk kwamba sheria hii ibadilishwe! Mtu ambaye amepatwa na ajali hata awe mhalifu ana haki ya kupata huduma ya kwanza!  Na mtu yeyote asibugudhiwe atakampomfikisha mtu aliyejeruhiwa hospitalini, bali waendelee kuchukua maelezo yake huku mgonjwa akiendelea kupata huduma ya kwanza. Okoa maisha kwanza! Suala hili mi binafsi nitalifuatilia lakini naamini ni jukumu letu sote kuhakikisha sheria hii inafutwa na badala yake uwekwe utaratibu mzuri ambao utathamini maisha ya mwananchi wa Tanzania, kuliko kesi ya polisi.