Kama kawaida, nilikuwa napata masimulizi ya hapa na pale
katika saluni – na nilisimuliwa jinsi mama daktari wa kujitolea mgiriki
alivyofariki dunia, jijini Dar, chanzo na mtiririko wa matukio.
Hii ni simulizi na si habari iliyothibitishwa. Kwa kifupi
mama huyu mgiriki alikuwa anatembea Ali Hassan Mwinyi Road na vibaka walipita
na gari na kuvuta begi lake la mgongoni (back pack) na kumburuza mita kadhaa na
gari. Hatimaye walichukua begin a kumwacha huyu mama. Sehemu hii imethibitishwa
– ni kweli ilitokea. Ila sasa nilichoendelea kusimuliwa ni kuwa wagiriki wenzake
walihangaika tokea saa 12jioni hadi saa 2 usiku wakijaribu kupata form ya polisi –
kwani bila hiyo fomu hupokelewi hospitalini. Walifika hospitali ya Aga Khan saa
2 lakini pamoja na kujitahidi kwa madaktari wenzake wagiriki (ambao waliamua
kuingia katika harakati za kumwokoa) lakini mama huyu alifariki.
Katika simulizi hii yote kilichonisikitisha ni kuwa mtu
anapopata ajali ni lazima apate fomu ya polisi kabla ya kutibiwa! Hii si sawa!
Nimewahi kushauriwa na polisi afisa mmoja na hata leo saluni walinishauri “Ukikuta mtu
kagongwa barabarani, usihangaike kusimama. Utasumbuliwa na unaweza ukakuta kesi
inakugeuka” Hii haiingi akilini! Hivi kweli tumefikia hatua ya kuacha binadamu
wenzetu wakivuja damu barabarani kwa sababu ya sheria mbovu? Hivi kweli tumeshindwa kushinikiza bunge, serikali nk
kwamba sheria hii ibadilishwe! Mtu ambaye amepatwa na ajali hata awe mhalifu
ana haki ya kupata huduma ya kwanza! Na mtu
yeyote asibugudhiwe atakampomfikisha mtu aliyejeruhiwa hospitalini, bali waendelee kuchukua maelezo yake huku mgonjwa akiendelea kupata huduma ya kwanza. Okoa maisha kwanza! Suala
hili mi binafsi nitalifuatilia lakini naamini ni jukumu letu sote kuhakikisha
sheria hii inafutwa na badala yake uwekwe utaratibu mzuri ambao utathamini
maisha ya mwananchi wa Tanzania, kuliko kesi ya polisi.