Mgomo huu wa madaktari wa mwaka 2012 ambayo sasa iko katika
awamu ya tatu imejadiliwa kwa kirefu na kwa kiina na wengi na mimi sitapenda
kutoa chanzo, sababu nk. Ila ningependa kuongelea mada moja ambayo
nimeshawahi kuigusia kwenye blog hii ya
IMHO inayohusu utawala wa walio wa kati au uwezo mdogo. Kwa kifupi wale wenye
ujuzi na uwezo huwekwa pembeni katika mfumo ambao upo sasa wa kiutawala na
uendeshaji kwa ujumla.
Lakini kibaya zaidi mufmo mzima unaonekana kutothamini usomi
na ujuzi. Tukiwasikiliza kwa makini madaktari, walimu na wasomi wengine –
tunasikia wakisema “sisi mshahara wetu ni …. Na mbunge ambaye hata hajamaliza
darasa la saba anapata milioni 10” Tunaweza kuleta mjadala mkubwa kuhusu
sentensi hii na kuwaita waroho, au tukawaambia hakuna kinachowasimamisha
kugombea ubunge. Lakini tukifanya hivyo tutakuwa hatujaelewa kile kilichojificha
katika sentensi hii.
Katika dunia ya leo hasa hapa nchini – tunaweka thamani ya
mtu kwa kupima kipato chake. Huu ni ukweli tupende tusipende. Mara ngapi
unasikia watu wanasema “Mtu anajiona wa maana kumbe anapanda daladala” . Au “Fulani
anajisikia, kumbe anaishi ….” Sentensi kama hizi zinaonyesha wazi kwamba ili
ukubalike kuwa una mafanikio katika jamii yetu tunatarajia mtu awe na gari na
anaishi maeneo Fulani, akivaa nguo za aina Fulani nk. Kwa kifupi jamii yetu
imebadilika na hivi sasa tumekuwa nchi ya walaji (Consumer society) ingawa kama
nchi hatuzalishi kile tunachotamani (hatuna viwanda vya magari, nguo, nk). Sasa
basi kumiliki gari, nyumba, mavazi etc yanahiitaji pesa. Hivyo kama daktari
anashindwa kuendesha Range Rover Vogue, lakini mfanyabiashara aliyeishia darasa
la saba akiweza, je hii ni kusema tutamheshimu zaidi mfanyabiashara? Inaelekea
ndivyo madaktari wanavyoona. Na kwa Bahati mbaya kwa kuwaambia “kama
hamjaridhika ondokeni” – imekuwa kama kuwathibitishia imani yao hii.
Ni vyema tukianza kuthamini watu kwa UJUZI wao na si kwa
MALI zao. Kumiliki gari kubwa au nyumba kubwa inaweza ikakufanya uishi kwa
starehe zaidi lakini haikuongezi akili au ujuzi. Na pia kama jamii tuache
dharau kwa watu. Hata kama mtu hamiliki mali nyingi, tuthamini vipaji, ujuzi na
elimu yao. Lakini muhimu zaidi, muda umefika mfumo wote uanze kuthamini kwa
pesa na kuwazawadia wale wenye ujuzi na si kuwajali ‘wajanja’.
Utatuzi wa mgomo huu na kutoridhika kwa wasomi ni suala
ambalo ni vyema sote tukaitafakari na tukianza kubadilika kimawazo – Change Tanzania!