Saturday, July 7, 2012

Mgomo wa madaktari na kuthaminiwa kwa wasomi


Mgomo huu wa madaktari wa mwaka 2012 ambayo sasa iko katika awamu ya tatu imejadiliwa kwa kirefu na kwa kiina na wengi na mimi sitapenda kutoa chanzo, sababu nk. Ila ningependa kuongelea mada moja ambayo nimeshawahi  kuigusia kwenye blog hii ya IMHO inayohusu utawala wa walio wa kati au uwezo mdogo. Kwa kifupi wale wenye ujuzi na uwezo huwekwa pembeni katika mfumo ambao upo sasa wa kiutawala na uendeshaji kwa ujumla.
Lakini kibaya zaidi mufmo mzima unaonekana kutothamini usomi na ujuzi. Tukiwasikiliza kwa makini madaktari, walimu na wasomi wengine – tunasikia wakisema “sisi mshahara wetu ni …. Na mbunge ambaye hata hajamaliza darasa la saba anapata milioni 10” Tunaweza kuleta mjadala mkubwa kuhusu sentensi hii na kuwaita waroho, au tukawaambia hakuna kinachowasimamisha kugombea ubunge. Lakini tukifanya hivyo tutakuwa hatujaelewa kile kilichojificha katika sentensi hii.
Katika dunia ya leo hasa hapa nchini – tunaweka thamani ya mtu kwa kupima kipato chake. Huu ni ukweli tupende tusipende. Mara ngapi unasikia watu wanasema “Mtu anajiona wa maana kumbe anapanda daladala” . Au “Fulani anajisikia, kumbe anaishi ….” Sentensi kama hizi zinaonyesha wazi kwamba ili ukubalike kuwa una mafanikio katika jamii yetu tunatarajia mtu awe na gari na anaishi maeneo Fulani, akivaa nguo za aina Fulani nk. Kwa kifupi jamii yetu imebadilika na hivi sasa tumekuwa nchi ya walaji (Consumer society) ingawa kama nchi hatuzalishi kile tunachotamani (hatuna viwanda vya magari, nguo, nk). Sasa basi kumiliki gari, nyumba, mavazi etc yanahiitaji pesa. Hivyo kama daktari anashindwa kuendesha Range Rover Vogue, lakini mfanyabiashara aliyeishia darasa la saba akiweza, je hii ni kusema tutamheshimu zaidi mfanyabiashara? Inaelekea ndivyo madaktari wanavyoona. Na kwa Bahati mbaya kwa kuwaambia “kama hamjaridhika ondokeni” – imekuwa kama kuwathibitishia imani yao hii.
Ni vyema tukianza kuthamini watu kwa UJUZI wao na si kwa MALI zao. Kumiliki gari kubwa au nyumba kubwa inaweza ikakufanya uishi kwa starehe zaidi lakini haikuongezi akili au ujuzi. Na pia kama jamii tuache dharau kwa watu. Hata kama mtu hamiliki mali nyingi, tuthamini vipaji, ujuzi na elimu yao. Lakini muhimu zaidi, muda umefika mfumo wote uanze kuthamini kwa pesa na kuwazawadia wale wenye ujuzi na si kuwajali ‘wajanja’.
Utatuzi wa mgomo huu na kutoridhika kwa wasomi ni suala ambalo ni vyema sote tukaitafakari na tukianza kubadilika kimawazo – Change Tanzania! 

1 comment:

  1. Maria, nakubaliana na wewe kabisa. 'Nchi' hii inakosa hekima. Tunaelekea kubaya. Miaka kumi ijayo itakuwa migumu sana kwa watanzania. Hekima inazidi kuwa bidhaa adimu na viongozi wetu hawaonekani kuwa wako makini. Juzi viongozi wa dini walitoa tamko, juzijuzi tena viongozi wa dini walizindua riport ya 'The billion dollar question'na kadhalika. Sijaona dalili yoyote ya usikivu kwa viongozi tuliowapa dhamana. Badala yake inatumika siasa kuchonganisha wanajamii. Shida ya sekta ya afya ni yetu sote na matatizo ni yetu sote. Madaktari ndio wanoguswa zaidi kwa sababu wako kwenye sekta hii muda wote. Wengine tunajihusha na sekta hii tukiumwa tu. Tukipona hatuna habari. Wanatueleza yanayoisibu sekta badala ya kuwasikiliza na kutafuta ufumbuzi wa pamoja tunawa-demonize.

    Nimeshuhudia wake za marafiki zangu wakifariki pale Muhimbili kwa matatizo yanayoweza kuepukika kabisa. Yametokea haya bila hata mgomo. Nimeshuhudia vijijini watu wanakufa tu nyumbani ndugu wameshakata tamaa kwamba hata ukienda hospitali hakuna tofauti. Tumeshuhudia mlolongo na misururu ya matajiri na maskini, wenye vyeo na wasio na vyeo, wakubwa kwa wadogo wakienda kupata kikombe cha babu. Hiyo ni dalili nyingine kuwa sote tumepoteza imani mfumo rasmi wa huduma za afya. Imefikia hata madaktari hatuwaamini. Si kwa sababu za kiueledi bali hakuna vifaa vya uchunguzi, hakuna madawa na kadhalika.

    Serikali ndio mdau mkuu, mawaziri wanasombana kwenda kunywa kikombe cha babu ni aibu kuu. Kutokujali kwa serikali ni dalili tu mojawapo ya kutokuthamini hii sekta kunakotokana na kukosa imani ya huduma ya wataalamu wetu. Niishie hapo!

    ReplyDelete