Katika mjadala unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba nilibahatika wiki
hii kupata nafasi ya kuchangia na nilizungumzia suala la ubabe wa walio wengi
au kwa kiingereza “Tyranny of the Majority”. Nilitumia hoja hii ya msingi
kuelezea kwa nini katika mchakato wa kurekebisha rasimu ya katiba tunahitaji
kura ziwe za siri. Ila kutokana na ufinyu wa muda sikupata nafasi ya kujieleza
kirefu na pia sikuwa na lengo la kuanzisha darasa kwa sababu mi si mwalimu wala
haikuwa nafasi yake hapo.
Hata hivyo nilimsikia siku inayofuata kaka yangu Peter Serukamba
akijaribu kujibu hoja yangu kwa kusema demokrasia ni ya wengi wape. Hii ni hoja
ambayo wajumbe wengine pia waliibua. Na imenisikitisha kwamba pamoja na wajumbe
hawa tumekusanyika nao katika bunge hili maalum la katiba na hawana uelewa mzuri
wa maana pana ya demokrasia. Hawaelewi kwa nini kuna wawakilishi wa asasi
zisizo za kiraia na vikundi vya kijamii katika bunge hili maalum la katiba ambao
kazi yetu ni kuwasemea watanzania wasiosikika – watoto, akina mama, walemavu,
wavuvi na kadhalika. Hawaelewi kwa nini rasimu yetu ya katiba ina haki za
binadamu na haki za raia. Kama demokrasia ingekuwa “wengi wape” tu, katiba yetu
ingekuwa ina ukurasa chache sana na tungeweza hata kuendelea kuwa na chama
kimoja na mgombea mmoja. Lakini sivyo ilivyo na sivyo watanzania tunavyotaka
kujenga nchi yetu.
Hoja yangu ya ubabe wa walio wengi huanzia kabla kura hazijapigwa na
baada ya kura kupigwa. Umuhimu wa kura ya siri ni kuwalinda wale ambao wanaweza
kutishiwa kwa njia moja ama nyingine yaani “protection from intimidation”. Lakini
pia kuna hoja ya kuwa ni haki ya msingi ya kila mtu yaani haki ya uhuru wa
mawazo na maoni. Kura ya siri inampa uhuru huu kila mtu. Lakini kwa mwonekano
wangu hoja zaidi ni kama wataalam wengi wanavyoshauri kuwa kura ya siri ni muhimu
pale ambapo uwezekano wa kutishiwa au kushurutishwa upo. Katika mazingira kama haya
basi ni njia mwafaka wa kupata maamuzi. Bila kupoteza muda ningependa kurudi
kwenye hoja wa “walio wengi” kwani hata dhana hii inabidi tuijadili zaidi.
Kusema wingi wa kura pekee ndo demokrasia ni mwonekano mfinyu. Hebu
nifafanue kidogo kwa faida ya wale ambao uelewa wao haujapanuka kwa nini
nimetoa tahadhari aliyoitoa James Madison na John Adams – moja wa vinara waliotunga
katiba ya Marekani - kuhusu ubabe wa walio wengi.
Hoja ya “walio wengi” (majority) si lazima iwe hoja yenye maslahi ya
taifa kutokana na ubinadamu wetu. Na John Adams alifafanua vyema maslahi haya
kuwa yanaweza kuwa maslahi ya familia zao, vitongoji vyao au vyama vyao. Hivyo
alisihi kuwa kuna haja ya kuweka vifungu katika katiba itakayotetea mfumo wa
haki, kuwalazimu wote kuheshimu maslahi ya pamoja na ya taifa dhidi ya maslahi
binafsi au ya kichama: “If a majority are
capable of preferring their own private interest, or that of their families,
counties, and party, to that of the nation collectively, some provision must be
made in the constitution, in favor of justice, to compel all to respect the common
right, the public good, the universal law, in preference to all private and
partial considerations”
Hivyo basi John Adams alisisitiza kuwa vifungu hivi vya katiba yaani
Bill of Rights ndivyo vitakavyomlinda mtu binafsi kutokana na kile kinachoitwa
ubabe wa walio wengi. Haki hizi ni pamoja na uhuru wa maoni, uhuru wa kupata
hifadhi, uhuru wa dini na kadhalika
Katika chapisho la “Federalist papers” maandiko yaliyokusanywa ya wale
vinara walioshiriki kutunga katiba ya Marekani, James Madison pia alionya na
kutoa hali halisi iliyokuwepo wakati huo katika siasa za Marekani. Alieleza ni
jinsi gani wananchi wengi wanalalamika kuwa serikali haziaminiki, na maslahi ya
umma yanawekwa pembeni kutokana na ushindani wa vyama vya kisiasa; na vitu
vinaamuliwa si kwa kufuata misingi ya haki na kulinda walio wachache au wasio
na sauti (minority), lakini kwa kufuata nguvu kubwa ya walio wengi wenye
maslahi binafsi.
“Complaints are everywhere heard from
our most considerate and virtuous citizens, equally the friends of public and
private faith, and of public and personal liberty, that our governments are too
unstable, that the public good is disregarded in the conflicts of rival
parties, and that measures are too often decided, not according to the rules of
justice and the rights of the minor party, but by the superior force of an
interested and overbearing majority.”
Na ndiyo maana hata James Madison alizungumzia umuhimu wa vifungu vya
katiba vitakavyolinda haki ya mtu binafsi yaani Bill of Rights.
Ni dhahiri kuwa hao “walio wengi” leo, kuna siku lazima watakimbilia
kutaka kulinda haki zao kwa mfano haki ile ya “kila mtu anastahili kuheshimiwa
na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake na familia yake na nyumbani
kwake, kutoteswa au kudhalilishwa na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na
mawasiliano yake binafsi”. Kila mmoja wa “walio wengi” atapigia kelele haki
zake binafsi kwa sababu kuna uwezekano mlio wengi mkawa wachache. Historia ina
mifano ya kutosha.
Hivyo basi huwa napenda kusema kuwa historia ina mengi ya kutufundisha
na wala tusidhani kuwa eti tumevumbua sisi demokrasia au suala la katiba. Kama tumeamua
kuwa Tanzania iwe nchi inayoheshimu demokrasia basi tufuate misingi yake na
tujikite kuelewa vyema misingi hii.
Ubabe wa “walio wengi” inategemea hao walio wengi ni kina nani na katika
mazingira gani. Je “walio wengi” ndani ya chombo maalum kinachoandika katiba
ndiyo kweli “walio wengi” Tanzania? Je hawa “walio wengi” wana wingi wa nini na
je tunaweza kuwaamini kuwa watakuwa na wingi huo siku zote? Je tunaweza kusema
kwa uhakika kuwa “walio wengi” wanasukumwa na maslahi ya umma na kila mmoja wao
ataheshimu siku zote msingi wa haki? Jibu ni hapana. Na si kwamba hawa “walio
wengi” sasa ni wabaya sana kuliko wengine lakini ukweli ni kuwa kama nilivyowahi
kusema katika siasa hakuna malaika wala shetani. Hivyo kama mchakato wa sasa wa
katiba mpya iko katika chombo ambacho kimetawaliwa na wanasiasa basi tujue hapo
tunatakiwa tuwe makini sana. Tujikite kutetea haki za wote na tuweke misingi itakayohakikisha
kuwa maslahi binafsi au ya kichama hayatawali.
Sasa kwa nini niliibua hoja hii ya ubabe wa walio wengi? Niliibua kwa
sababu kabla hata hatujaanza mjadala kuhusu rasimu ya katiba, tukiwa bado
tunajadili rasimu ya kanuni zitakazotuendesha, ubabe huu umeonekana na ni
hatari kwa mustakabli wa taifa. Kwani inaashiria kuwa ubabe huu utaendelezwa
mpaka kwenye mijadala ya hapo mbele kuhusu rasimu ya katiba bila kuelewa vyema
kilichotuleta pamoja hapa Dodoma.
Hivyo kwa mtazamo wangu, walio wengi wasijitetee na wasitake kutushawishi kuwa ni
malaika, na mimi binafsi pamoja na wengine hata tusipokuwa na mitazamo
iliyofanana nao tusitake kuwafanya “walio wengi” ni waovu, ila tutambue hali
halisi na tufuate misingi ya demokrasia.
Kwa kumnukuu Edmund Burke mwanasiasa na mwanafalsafa wa Uingereza: “the
greater the power, the more dangerous the abuse” yaani jinsi nguvu inavyozidi
kuwa kubwa ndivyo dhuluma inaongezeka. Basi nguvu ya walio wengi isiwe ya ubabe
na dhuluma, bali iwe ni nguvu ya kweli na yenye kujitambua inayotaka kujenga
utaifa na kujali raia wote na haki zao. Kama msanii wa kifaransa, Paul Cezanne
alivyosema “the awareness of our strength makes us modest” yaani kutambua nguvu
tuliyo nayo hutufanya tuwe wa kawaida au kujishusha. Mtu mwenye nguvu ya kweli
na anayejitambua kamwe hawezi kuwa mbabe na siku zote hutafuta njia ya kuwasaidia
wasio na nguvu. Si kwa sababu ya huruma, lakini kwa sababu anaelewa nguvu yake
imetokana na nini. Hawa “walio wengi” leo
watakapopata jibu kuwa nguvu yao imetokea wapi wataelewa kuwa misingi hii ya
demokrasia na utaratibu tunajijengea sote kwa sababu hata kama si leo au kesho
lakini hatimaye mpanda ngazi hushuka.
Dear Maria.
ReplyDeleteYou have expressed your thoughts well. I do respect them.
But i have a question for you. Why are you pessimistic? What makes you to think someone will infringe the rights of the other who have different opinion than him or her?
And yes i have read the article and i appreciate your concerns. But when you think carefully about them you find that your "ideas" are influenced by one thing "you think pessimistic and not optimistic". You have developed the so called "self fulfilling prophecy". Your conclusion "kura za siri ndio suluhisho" is opposing democracy itself.
Hilo ni bunge la Katiba, kila kitu kiwe wazi. Watanzania tupo nyuma yenu. Tunataka tusikie kwa uwazi kabisa "nani katoa maoni gani, kapiga kura kuchagua nini na hiyo kura yake imetoa maamuzi ku-support upande upi.
Daniel.
Albanation
DeleteLaiti ungesoma vizuri hoja ya dada Maria ungemwelewa anachosema.
Maria ni mtu very OPTIMISTIC! Dhana ya "majority rule" ni dhana ambayo kama akina John Adams walivyosema, karne nyingi zilizopita, ni kwamba si lazima hoja za "wengi wape" ziwe na manufaa kwa taifa.
Mara ngapi tumesikia watu wakifukuzwa kazi au kutendewa kinyume na haki KWA KUWA TU walipigia kura chama fulani dhidi ya chama tawala, au hata walihisiwa kufanya hivyo? Unadhani huo UWAZI unaoutaka wewe utakuwa na maslahi gani kwa taifa iwapo hao watakaojulikana kupiga kura KINYUME na utashi wa hiyo "majority" watakapobainika?
Kila siku KURA HUWA NI SIRI ya mpiga kura. Bunge ambalo umelizoea la NDIYOOOOO au SIYOOOO si Bunge la Kidemokrasia, ni la KIDOMOKRASIA. Ndio maana Wamarekani waliachana na mfumo huo wa Kiingereza na kuweka mfumo ambao inaonekana ni WATU WANGAPI (sio WATU GANI) wamepigia kura hoja iliyopo mezani. Mfumo wa Marekani ni wa WAAZI ZAIDI kwani inaonekana ni WATU WANGAPI wamepiga kura, wangapi wamepiga kura ya NDIYO, wangapi wamepiga ya HAPANA, na wangapi HAWAKUPIGA.
Unapotaka kumjua ni NANI aliyepiga kura, unaonesha nia yako ya kutaka kumdhuru KWA KUWA TU hakukubaliana na hoja yako. Hapo unaenda kinyume na misingi ya demokrasia. Wapiga kura lazima walindwe na madhara ambayo watayapata kwa kuwa na msimamo tofauti, hapa tunazungumzia uhuru wa kikatiba, wa kuwa na maoni tofauti, uchaguzi tofauti, maamuzi tofauti, n.k.
Suala kusema kwamba ijulikane ni watu gani waliopigia kura hoja fulani, wakasema NDIYO au HAPANA, ni kinyume sana na demokrasia, HASWA KWENYE BUNGE LA KATIBA!
Usiturudishe nyuma kwenye zama za UJIMA wa kidhalimu ambapo suala la ZIDUMU FIKRA ZA MWENYEKITI zilitawala, jambo ambalo hata Mwalimu alilishtukia na kuliondoa, akitambia kwamba ulikuwa udikteta na si demokrasia.
LABDA UNAPENDA AMRI ZITOLEWE KILA UCHAO kwamba watu warukeruke kichura kila asubuhi, hata kama kufanya hivyo ni hatari kwa maisha yao, kwa kuwa tu MKULU amesema, na walio wengi - wenye maslahi naye - wanakubaliana naye, na wale wachache hawapendi kurushwa kichura kwa kuwa afya zao na mambo mengine hayawaruhusu kufanya hivyo?
Kaka, hebu rudi darasani kwanza, ukajifunze nini maana ya dhana nzima ya demokrasia.
Maria, watu kama hawa WASIKUCHOSHE! Msimamo ndio huo! Tuachane na demokrasia - DOMOKRASIA! - ya wababe walio wengi!
ALAMSIKI!
This comment has been removed by the author.
DeleteNdugu yangu Paul Francis Mongi, habari yako!
DeleteNimetumia neno "pessimistic" sio kuonyesha dada Maria hajui anachosema. Anajua vizuri tu, tene hiyo ndi sababu anatuwakilisha kwenye bunge la Katiba.
Nimetumia neno hili "pessimistic kwa sababu ukiangalia mtiririko mzima wa hoja yake unajegwa na kumbukumbu ya historia mbaya ya ukiukwaji wa haki za "minority".
Nashukuru kunikumbusha kuhusu John Adams. Nawewe pia ni vema ukasoma kitu kinachoitwa "Sociological Imagination by C Wright Mills 1959". Nadhani hapa utapata uelewa wa kujua point yangu imeegemea wapi.
Narudia tena zipo sababu muhimu sana za kufanya mchakato wa upigaji kura ndani ya Bunge la Katiba uwe wa wazi. Sababu zenyewe hizi hapa.
1.Hakuna sababu ya msingi ya usiri; kinachojadiliwa kinajulikana hoja ni kukubali au kukataa kilichojadiliwa au kinachopendekezwa. Kwanini iwe siri kukataa ibara au kifungu kibaya au kukikubali?
2. Asilimia zaidi ya themanini walioko kwenye Bunge la Katiba ni wabunge au wawakilishi; wengi wa hawa bila ya shaka watataka kugombea tena 2015. Sasa kwanini wananchi wasipate nafasi ya kujua wanasimamia wapi katika mambo ya msingi ya taifa. Hii ni nafasi ya pekee kwa Watanzania kujua viongozi wao wanasimaia wapi. Hata wale ambao si wabunge sasa wengine wanaweza kutaka kugombea; iwe wazi wajulikane mitazamo yao kisiasa na hakuna kipimo cha dhamira kama kupiga kura ya wazi. Kama wanaamini wanachokiamua hawana sababu ya kuwaficha wapiga kura.
3. Rasimu ya Katiba kutoka Tume ya Kina Warioba (Warrioba Commission) ina mambo mengi mno; ina mambo mengine hata hayaingii kichwani sijui walikuwa wanataka kufanya nini. Binafsi naamini kuna baadhi ya mambo hayapaswi kuwa sehemu ya Katiba yanatakiwa yawe kwenye sheria. Bahati mbaya rasimu hii – kwa makosa makubwa – imejaribu kuwa sheria na kujaribu kujaza kila kinachofikirika humo humo ndani. Mifano yake ipo mingi. Katiba inatakiwa kuweka kanuni za msingi, na kuacha Bunge kutunga sheria au vyombo vingine kutengeneza taratibu za kutii matakwa ya Kikatiba. Hivyo, ni muhimu wabunge wa Bunge la Katiba waonekane wazi wanasimamia wapi kwenye haya mambo mengi ambayo yote yatatusaidia siyo tu kujua misimamo ya watu lakini kuweza kuwahoji huko mbeleni.