Wednesday, December 9, 2015

#UnokoNiUzalendo – Unoko, ubahili, ushamba oyee!

Nilikuwa najaribu kuangalia tafsiri ya neno “mnoko”. Usishangae maana neno “mshamba”ninahisi nina tafsiri yake ya “country bumpkin” ingawa Google inasema ina maana ya “lout” ila inaweza kuwa na tafsiri ya ziada inapotumika leo hii Tanzania aka Bongoland. Alafu neno “mbahili” pia tafsiri inaeleweka “miser”. Nilikuwa natafuta tafsiri ya ‘mnoko’ ili nijaribu kumwelewesha mtu yeyote ambaye si mtanzania na haongei Kiswahili ni jinsi gani maneno haya yalitumika kama njia ya kuua uzalendo na maadili na kutukuza maisha yasiyo halisi. Hoja yangu ni kwamba leo hii, Unoko ni uzalendo, ubahili ni maendeleo, ushamba ni sifa.

Katika kampeni ya 2015, nilikuwa ninatazama na kusoma zaidi ya kuandika, hii ilikuwa ni sehemu ya kujaribu kuelewa nini kinasukuma watu kumpigia kura mgombea fulani au fulani. Kitu nilichokiona kinarudiwarudiwa ni neno “mshamba” wakati wa kumkosoa mgombea wa CCM, ambaye sasa ni Rais Magufuli. Nikaamua nisome zaidi maoni haya. Inaelekea kutosomesha watoto nje na katika shule za ‘academy’ ni ushamba, kutosafiri sana nje ni ushamba, na jinsi anavyovaa na lafudhi yake nzito pia inashiria kuwa ni mshamba. Lakini tusiwahukumu walioyasema hayo. Ni sawa kabisa kwamba katika jamii yetu ya sasa ambapo tumetilia mkazo muonekano wa nje wa mtu, neno ‘ushamba’ hapa linahusika. 
Rais Magufuli (archive)

Cha ajabu pamoja na ushamba huu, Rais Magufuli sasa anaonekana kweli ni mtu simple ambaye ameishi maisha halisi ya mtanzania na hahitaji kuigiza au kuvaa mara moja moja kama mtu wa kawaida. Ndivyo alivyo. Na tunaanza kuona kuwa wale waliokuwa wanabadili magari kila kukicha na wanamiliki nyumba 73 walikuwa hawaishi maisha ya kweli kwani walikuwa wanavunja sheria. Nadhani muda si mrefu ushamba utakuwa ni sifa na kila mtu atataka awe ‘mshamba’ asiyejua ujanja wa teni pasenti.

Kwenye ubahili ninakumbuka wakenya walianzisha hashtag #WhatWouldMagufuliDo na mwanzoni baadhi ya watanzania huko Twitter waliona kama wanamkejeli Rais maana hata picha na tweets ziliashiria ubahili wa kupitiliza. Lakini muda si mrefu, hashtag ikawa maarufu na hivi sasa wanahabari, wanaharakati na watoa maoni wa nchi mbalimbali wanashauri serikali na viongozi wao kuwa bora wawe kama Magufuli – yaani wajali sana matumizi. So ubahili sasa umekuwa ni suala la maendeleo!
Rais Magufuli akiwa chuo kikuu

Mwisho kabisa narudi kule nilipoanza kuhusu unoko! Ah! Neno “mnoko”! Ukiitwa mnoko shule lazima ulie! Ina maana wewe ni yule ambaye utawasemea wenzako wanaopiga kelele, utanyoosha kidole wa kwanza kujibu swali, mkiambiwa mkafanye usafi utakuwa wa kwanza kupanga mstari na fagio lako na utavaa sare zako safi kila siku bila kukosa. Na bila shaka utakuwa unakaa mstari wa mbele shuleni na unajitahidi kusoma uwe unaongoza darasani, ukikosa maksi uliyokusudia kidogo unalia. Sasa ukishaingia miaka ile ya kuanza kupevuka kimwili, unoko haukuwa sifa nzuri. Maana wanoko hawakupendwa na hawakuvutia. 


Baada ya masomo, kama mtu mzima kama uliendelea kuwa mnoko utaonekana mbaya kwa majirani, wafanyakazi wenzako na hata bosi wako. Wanoko hawapandishwi cheo na ni nadra wao kuonekana na viongozi wao na kuchaguliwa kuongoza. Ingawa wanoko wengi ni viongozi wa asili. Wanataka vitu viende vizuri kwa manufaa ya wengi, kila mtu afuate sheria hata ye na familia yake, na tuheshimiane wakubwa kwa wadogo. Kwa maelezo haya, nahisi sitakosea kusema Rais Magufuli ni mnoko. Yaani vijana wanasema, “Dah! Huyo ka Dingi wako basi atakuwa mnoko!”. Lakini leo hii hakuna anayelalamikia unoko huu wa Rais Magufuli. Ghafla wote tunasema ni muhimu sheria zifuatwe, tujenge taifa, tusimamie na tushirikiane usafi siku ya Uhuru na muhimu ‘kumsemea’ anayevunja sheria, haya yote ni vitu vizuri. Sasa tunasema Unoko ni Uzalendo.
Kwa kumalizia ni hivi, naamini kuwa ni wachache ndiyo walituaminisha kwamba eti ukitaka kusimamia haki, ufuataji wa sheria, kusimamia matumizi mazuri na sahihi binafsi au ya serikali au kuhamasisha jamii basi wewe ni mnoko. Ni wachache ambao walitaka tuamini eti Tanzania ya leo ni aibu au ushamba kutomiliki gari hata kama wewe ni binti wa miaka 20 na hatua pekee uliyopiga maishani ni kushinda mashindano ya urembo. Ni wachache waliotuaminisha kuwa usipofanya sherehe kubwa ya harusi basi ni mbahili au mshamba. Lakini watanzania tulio wengi tulikaa kimya. Tuliendeshwa kwa kiasi lakini wengi tulibaki watazamaji zaidi na tulikubali kuwekwa katika kundi hilo la washamba, wabahili na wanoko. Tulikuwa tunasubiri siku ambapo kejeli hizi zitageuka kuwa sifa.

1 comment:

  1. Those who satand for the Truth always stand allone nimeipenda sana site hii inaleta hamasa kuwa ktk page hii tofauti na site nyingi watanzanioa wengine hupenda sana kupoteza muda ktk mada zakipuuzi while tunaishi maisha yakuungaunga lazima tuende na ukweli this site mostly i am very impressed to join.its our right time to move constructively and walk in positive way.nakutakia kazi njema stay blessed SARUNGI.

    ReplyDelete