Huwa tumezoea kusikia kuwa Mabadiliko ni mimi, ni wewe
(Twaweza.org), ya kuwa tunatakiwa tuwe chachu ya Mabadiliko. na - tokea 2008,
baada ya kampeni na ushindi wa Obama – ‘Mabadiliko huanza na wewe’.
Cha ajabu ingawa tunarudiarudia sana maneno haya na
kuyasikia, bado kama Taifa na wananchi, sisi watanzania tunasubiri mabadiliko
YALETWE na mtu au kikundi cha watu. Tunamsubiri Nabii wetu wa Mabadiliko,
tunamtafuta Obama wetu wa 2008. Wengine wanasubiri Nyerere mwingine au Sokoine
mwingine. Tunasubiri Nabii huyu ajitambue, azinduke, apate nguvu na ujasiri,
ajitokeze na kisha atuongoze .. kuelekea wapi hatujui ila tusibaki hapa tulipo.
Hii ndo hali halisi na tupo tayari kuijengea hoja tena kwa
nguvu na kutetea hali hii. Utamsikia msomi anayekaa mjini akisema, “Tatizo letu
sisi watanzania wengi ni maskini..” “Tatizo ni mfumo wetu wa elimu” na
tunachopenda kurudia sana sote ni: “Ujinga wa watanzania ndo mtaji wa viongozi wetu
wabovu” Utamsikia mwenyekiti wa jumuiya ya kijamii (al maarufu kama CBOs yaani
Community Based Organizations) akilalama, “Tunahitaji kuwezeshwa”. Wapo
wanaosema “Wewe umefanya nini?” kana kwamba kutofanya kitu kwangu ndo sababu nao kukaa tu kusubiri kuletewa mabadiliko. Basi tu sababu lukuki. Mfano mzuri ni jinsi tulivyojaribu Change
Tanzania kuhamasisha watu tukusanye sahihi kutaka uwajibikaji kamili katika
kesi ya Tegeta Escrow. Wapo wanaohoji, “Itasaidia nini? Haisaidii kitu.” Basi
tuendelee kukaa tu?
Ninawaheshimu sana na kuwapongeza wanaochangisha jamii
kununua madawati, kujenga mashule, kuelimisha watoto nk kwani hata kama ni
watoto wawili tu wananufaika na juhudi zao, ni hatua kubwa kuliko kutofanya
kitu na kulalama. Tatizo tunalolifahamu sote ni kuwa bila mfumo mzuri wa
utawala, misaada hii ni tone la maji katika bahari. Lakini juhudi zote ni
muhimu tusizibeze.
Kwani tukibeze juhudi hizi ndogo na tukikubali kuwa sisi
watanzania ni maskini, wajinga na tuna maradhi chungu mbovu.. swali ni je, kwa
hiyo tuendelee kusubiri Nabii ajitokeze miongoni mwetu ambaye hatakuwa mjinga,
maskini na atakuwa buheri wa afya?
Kwa leo sitaki kuingia katika suala la vyama vya siasa au
kutaja majina ya viongozi, ninachotaka kufanya ni kuwachokoza watanzania
wenzangu, hivi wenzangu hamjachoka? Mi naona hakuna Mkombozi atakayeshushwa
kutoka mbinguni. Hakuna Sauti ya Mungu itakayosikika hadharani ikitupa mwongozo
tufanyeje, kwa sababu sote tulipewa dira (compass) mioyoni mwetu na Mungu. Hiyo
dira inatakiwa ituongoze na kutupa mwelekeo. Dira yangu inaniambia tupo njia
isiyo sahihi kama nchi. Kama taifa tumekosa uadilifu, nidhamu, utu na upendo
kwa binadamu wenzetu. Tumekuwa nchi iliyokata tamaa. Lakini naamini kukata
tamaa ni kosa na nina matumaini kuwa kila mmoja wetu alizaliwa mtanzania kuishi
mwaka huu na nyakati hizi kwa sababu tumepangiwa kazi. Hivi ndivyo Nyerere,
Sokoine, Gandhi, Mandela na wanamabadiliko mashuhuri walivyofikiri. Waliamini
hawakuzaliwa katika mazingira yao kwa bahati mbaya. Tuko hapa duniani kwa
malengo makubwa zaidi ya kupata mkate wa kila siku.
Kila mmoja wetu akitambua hili, ndipo Taifa litazinduka na
ndipo tutaona kuwa nchi itageuzwa na mabadiliko yatatokea. Na watu wa mataifa
mengine na wanahistoria watajaribu kutafuta mashujaa wa kuwapa sifa zote na
kuwatunuku nafasi hii ya kinabii, bila kutambua kuwa mabadiliko haya yaliletwa
na kila mmoja wetu na kila mtanzania. Hii labda ni ndoto, achene niote tu..
bora niendelee kuota kuliko kukata tamaa na kukaa kuangalia mbinguni nikisubiri
kishushiwa Nabii wa mabadiliko.
No comments:
Post a Comment