Nilikuwa najaribu kuangalia tafsiri ya neno “mnoko”.
Usishangae maana neno “mshamba”ninahisi nina tafsiri yake ya “country bumpkin”
ingawa Google inasema ina maana ya “lout” ila inaweza kuwa na tafsiri ya ziada
inapotumika leo hii Tanzania aka Bongoland. Alafu neno “mbahili” pia tafsiri
inaeleweka “miser”. Nilikuwa natafuta tafsiri ya ‘mnoko’ ili nijaribu
kumwelewesha mtu yeyote ambaye si mtanzania na haongei Kiswahili ni jinsi gani
maneno haya yalitumika kama njia ya kuua uzalendo na maadili na kutukuza maisha
yasiyo halisi. Hoja yangu ni kwamba leo hii, Unoko ni uzalendo, ubahili ni
maendeleo, ushamba ni sifa.
Katika kampeni ya 2015, nilikuwa ninatazama na kusoma zaidi
ya kuandika, hii ilikuwa ni sehemu ya kujaribu kuelewa nini kinasukuma watu kumpigia
kura mgombea fulani au fulani. Kitu nilichokiona kinarudiwarudiwa ni neno
“mshamba” wakati wa kumkosoa mgombea wa CCM, ambaye sasa ni Rais Magufuli.
Nikaamua nisome zaidi maoni haya. Inaelekea kutosomesha watoto nje na katika
shule za ‘academy’ ni ushamba, kutosafiri sana nje ni ushamba, na jinsi
anavyovaa na lafudhi yake nzito pia inashiria kuwa ni mshamba. Lakini
tusiwahukumu walioyasema hayo. Ni sawa kabisa kwamba katika jamii yetu ya sasa
ambapo tumetilia mkazo muonekano wa nje wa mtu, neno ‘ushamba’ hapa linahusika.
Rais Magufuli (archive) |
Cha ajabu pamoja na ushamba huu, Rais Magufuli sasa anaonekana kweli ni mtu
simple ambaye ameishi maisha halisi ya mtanzania na hahitaji kuigiza au kuvaa
mara moja moja kama mtu wa kawaida. Ndivyo alivyo. Na tunaanza kuona kuwa wale
waliokuwa wanabadili magari kila kukicha na wanamiliki nyumba 73 walikuwa
hawaishi maisha ya kweli kwani walikuwa wanavunja sheria. Nadhani muda si mrefu
ushamba utakuwa ni sifa na kila mtu atataka awe ‘mshamba’ asiyejua ujanja wa
teni pasenti.
Kwenye ubahili ninakumbuka wakenya walianzisha hashtag
#WhatWouldMagufuliDo na mwanzoni baadhi ya watanzania huko Twitter waliona kama
wanamkejeli Rais maana hata picha na tweets ziliashiria ubahili wa kupitiliza.
Lakini muda si mrefu, hashtag ikawa maarufu na hivi sasa wanahabari,
wanaharakati na watoa maoni wa nchi mbalimbali wanashauri serikali na viongozi
wao kuwa bora wawe kama Magufuli – yaani wajali sana matumizi. So ubahili sasa
umekuwa ni suala la maendeleo!
Rais Magufuli akiwa chuo kikuu |
Mwisho kabisa narudi kule nilipoanza kuhusu unoko! Ah! Neno “mnoko”!
Ukiitwa mnoko shule lazima ulie! Ina maana wewe ni yule ambaye utawasemea
wenzako wanaopiga kelele, utanyoosha kidole wa kwanza kujibu swali, mkiambiwa
mkafanye usafi utakuwa wa kwanza kupanga mstari na fagio lako na utavaa sare
zako safi kila siku bila kukosa. Na bila shaka utakuwa unakaa mstari wa mbele
shuleni na unajitahidi kusoma uwe unaongoza darasani, ukikosa maksi
uliyokusudia kidogo unalia. Sasa ukishaingia miaka ile ya kuanza kupevuka kimwili,
unoko haukuwa sifa nzuri. Maana wanoko hawakupendwa na hawakuvutia.
Baada ya
masomo, kama mtu mzima kama uliendelea kuwa mnoko utaonekana mbaya kwa
majirani, wafanyakazi wenzako na hata bosi wako. Wanoko hawapandishwi cheo na
ni nadra wao kuonekana na viongozi wao na kuchaguliwa kuongoza. Ingawa wanoko
wengi ni viongozi wa asili. Wanataka vitu viende vizuri kwa manufaa ya wengi,
kila mtu afuate sheria hata ye na familia yake, na tuheshimiane wakubwa kwa
wadogo. Kwa maelezo haya, nahisi sitakosea kusema Rais Magufuli ni mnoko. Yaani
vijana wanasema, “Dah! Huyo ka Dingi wako basi atakuwa mnoko!”. Lakini leo hii
hakuna anayelalamikia unoko huu wa Rais Magufuli. Ghafla wote tunasema ni
muhimu sheria zifuatwe, tujenge taifa, tusimamie na tushirikiane usafi siku ya
Uhuru na muhimu ‘kumsemea’ anayevunja sheria, haya yote ni vitu vizuri. Sasa
tunasema Unoko ni Uzalendo.
Kwa kumalizia ni hivi, naamini kuwa ni wachache ndiyo
walituaminisha kwamba eti ukitaka kusimamia haki, ufuataji wa sheria, kusimamia
matumizi mazuri na sahihi binafsi au ya serikali au kuhamasisha jamii basi wewe
ni mnoko. Ni wachache ambao walitaka tuamini eti Tanzania ya leo ni aibu au
ushamba kutomiliki gari hata kama wewe ni binti wa miaka 20 na hatua pekee
uliyopiga maishani ni kushinda mashindano ya urembo. Ni wachache
waliotuaminisha kuwa usipofanya sherehe kubwa ya harusi basi ni mbahili au
mshamba. Lakini watanzania tulio wengi tulikaa kimya. Tuliendeshwa kwa kiasi
lakini wengi tulibaki watazamaji zaidi na tulikubali kuwekwa katika kundi hilo
la washamba, wabahili na wanoko. Tulikuwa tunasubiri siku ambapo kejeli hizi
zitageuka kuwa sifa.
Those who satand for the Truth always stand allone nimeipenda sana site hii inaleta hamasa kuwa ktk page hii tofauti na site nyingi watanzanioa wengine hupenda sana kupoteza muda ktk mada zakipuuzi while tunaishi maisha yakuungaunga lazima tuende na ukweli this site mostly i am very impressed to join.its our right time to move constructively and walk in positive way.nakutakia kazi njema stay blessed SARUNGI.
ReplyDelete